MSICHANA Dorika Kanomba (18) amehukumiwa kifungo cha mwezi mmoja jela au kulipa faini ya Sh 150,000 baada ya kukiri kosa la kukutwa akifanya biashara haramu ya kuuza mwili. Washitakiwa wengine tisa waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive kwa kosa hilo, wamerejeshwa mahabusu baada ya kukana mashitaka yanayowakabili.
Akitoa
hukumu jana, Hakimu wa mahakama hiyo, Said Mkasiwa alisema Dorika
atatumikia kifungo cha mwezi mmoja jela au kulipa faini hiyo baada ya
kukiri makosa.
Mwendesha
Mashitaka wa Serikali, Richard Magodi aliwataja washitakiwa wengine
waliofikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na kosa hilo kuwa ni Veronika
Benjamini (17), Nasra Ismail (18), Mary Gerard (16), Milka Braun (17),
Fatuma Ally (22), Alice Samweli (17), Farida Hemed (20), Anitha James
(18) na Martha Mange (20).
Magodi
alidai kuwa Novemba 29, mwaka huu eneo la Manzese wilayani Kinondoni,
washitakiwa hao walikutwa wakifanya biashara haramu ya kuuza miili,
maarufu kama ukahaba, kinyume cha maadili.
Washitakiwa tisa walikana mashitaka hayo ambapo Dorika alikiri na kuhukumiwa kifungo cha mwezi mmoja au kulipa faini.
Mahakama
ilitoa nafasi ya dhamana kwa washitakiwa kwa masharti ya kulipa Sh
160,000 kwa kila mmoja, lakini hawakutimiza masharti hayo. Kesi hiyo
itatajwa tena Desemba 10, mwaka huu.
Wakati
huo huo, wanawake wawili Zainabu John (28) na Hamida Masoud (43),
wamehukumiwa kifungo cha siku 21 jela au kulipa faini ya Sh 120,000
baada ya kukutwa wakiuza bidhaa maeneo yasiyohusika kinyume cha sheria.
Akitoa
hukumu hiyo jana, Hakimu Said Mkasiwa alisema akina mama hao
watatumikia kifungo cha siku 21 jela au kulipa faini ya Sh 120,000 baada
ya kukiri kufanya biashara hizo kinyume cha sheria.
Mwendesha
Mashitaka wa Serikali, Richard Magodi alidai kuwa Novemba 29, mwaka huu
katika eneo la Vingunguti, washitakiwa hao walikutwa wakiuza bidhaa
katika maeneo yasiyoruhusiwa kinyume cha sheria.
-Habari leo
-Habari leo