MWENYEKITI wa CCM Kijiji cha Chole wilayani Kisarawe, Pwani, Kondo Shamte (36) yuko katika hali mbaya baada ya kuchomwa mkuki tumboni na wafugaji wa kabila la Wamang’ati na kusababisha utumbo wake kuwa nje.
Kwa
mujibu wa mwenyekiti huyo ambaye kwa nafasi yake kijijini hapo ndiye
anayeheshimika zaidi, tukio hilo lilijiri Agosti 28, mwaka huu.
Akizungumza
kwa masikitiko makubwa nyumbani kwake kijijini hapo, Kondo alisema
katika kijiji hicho kulijengwa barabara na wahisani (hakuwataja jina).
Wanakijiji wakaombwa kuitunza barabara hiyo kwa masharti kwamba
wasipitishe mifugo.
Alisema
siku ya tukio, wafugaji hao walipitisha mifugo katika barabara hiyo
licha ya amri iliyokuwepo, alipoona hali hiyo aliwafuata na kuwaomba
wapitishe pembeni.
“Walikataa,
nikaamua kuwatuma wajumbe wangu wawafuatilie kwa nyuma ili wasiendelee
kupitisha mifugo hiyo,” alisema mwenyekiti huyo.
Akaendelea:
“Baada ya wafugaji hao kuona nimetuma wajumbe wakarudi hadi nilipokuwa
nimesimama na kuniambia kuwa niliwatuma wale wajumbe ili wakawafanyie
fujo, wakatoa vitisho kwamba ule ndiyo ungekuwa mwisho wangu.
Mwenyekiti
huyo aliendelea kusema kuwa kabla yeye hajazungumza chochote, mfugaji
mmoja alichomoa mshale na kumrushia ambapo ulimwingia tumboni kisha wote
wakakimbia.
Alisema
alijitahidi sana kuutoa mshale huo huku tayari akiwa ameanguka chini.
Alipofanikiwa, ndugu na jamaa nao walitokea na kumkimbiza Hospitali ya
Kisarawe.
“Pale
hospitalini Kisarawe ilishindikana kunitibu, nikakimbizwa Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (Dar es Salaam) ambako nilifanyiwa upasuaji mkubwa
kwa kukata sehemu ya utumbo iliyoharibika,” alisema.
Mwenyekiti
huyo aliendelea kuweka wazi kwamba baada ya operesheni hiyo daktari
alimwambia ni lazima sehemu ya utumbo utolewe nje mpaka sehemu ya ndani
ipone vizuri ndipo waurudishe, hivyo kwa sasa haja kubwa anaitolea
ubavuni.
“Hivi sasa haja kubwa natolewa kwa hapa ubavuni mpaka nitakaporudi tena hospitali mwezi Desemba, mwaka huu,” alisema.
Hata
hivyo, Kondo alisema kitu kinachomuuma zaidi ni kutomuona kiongozi wa
CCM hata mmoja aliyefika nyumbani kwake kumjulia hali wala kumpa msaada
wowote kwani hivi sasa yuko katika hali ngumu ya kimaisha kutokana na gharama za kutibu kidonda chake kuwa juu.