Mwenyekiti wa Chama Chama Mapinduzi (CCM),Febronia Ikombe.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi nyumbani kwake baada ya kutoka hospitali alikokuwa akitibiwa, Ikombe alisema siku ya tukio alipokea taarifa kutoka kwa wakazi wa Kijiji cha Kanegele kwamba kuna ng’ombe wameingia shambani kwake.
Ikombe alisema aliondoka na kwenda shambani akiongozona na watoto wake watatu na dereva wake. Walipofika walikuta ni kweli ng’ombe hao wakiwa shambani. Alisema kutokana na hali hiyo aliwafuata wachungaji wa mifugo hiyo na kuwahoji kwa nini wameingiza mifugo shambani mwake.
Alisema hakupewa jibu, badaka yake mmoja wa wachungaji aliyejulikana kwa jina moja la Mwanasabuni alipiga mayowe hali iliyomshangaza Ikombe.
“Mara niliona kundi la wanakijiji wakija shambani hapo wakiwa na silaha za jadi, fimbo, mapanga na marungu, nilishtuka sana, nikamuuliza Mwanasabuni kwa nini amepiga mayowe, hakunijibu,” alisema.
Alidai wananchi hao baada ya kufika walimshambulia kwa kuwapiga yeye na watoto wake wakitumia fimbo ambapo waliwajeruhi.
“Nimepasuka sehemu ya kushoto karibu na jicho, nilizinduka nikiwa hospitalini ambako nilishonwa nyuzi sita. Mtu aliyenipiga namkumbuka ni mgeni wa mwana kijiji cha Kanegele. Kwa kweli imenisikitisha sana,” alisema mwenyekiti huyo.