Mwanafunzi aliyehitimu kidato cha nne mwaka huu, Sharifa Abdallah (18) ameuawa kwa kuchomwa kisu shingoni na mbavuni chumbani kwa mvulana aliyedai kuwa mpenzi wake maeneo ya Kimara Golani, Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 8:30 mchana na baadaye mvulana huyo aliyetambuliwa na Polisi kwa jina la Abdul Alpha (22) kujisalimisha katika kituo cha Polisi cha Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo, akidai alikuwa akitaka kutoroka lakini aliona amefanya dhambi kubwa.
Akizungumza
na mwandishi jana, mama mkubwa wa marehemu, Mwajuma Khamis alisema
Sharifa alimaliza kidato cha nne katika sekondari ya Luguruni na alikuwa
akisubiri matokeo.
Alisema
juzi waliporejea kutoka kazini hawakumkuta nyumbani, waliulizia kwa
ndugu kutokana na kwamba hakuwa na tabia ya kutoka nyumbani, lakini
hawakufanikiwa kumpata hadi jioni ndipo polisi walipowataarifu
kupatikana kwa mwili wake.
Alisema
mwili wa marehemu ulikutwa chumbani kwa kijana huyo karibu na nyumbani
kwao ukiwa na majeraha mwilini, lakini hawakujua kama mtoto wao ana
mwanaume, wanatarajia kumzika kesho saa saba mchana.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema polisi
walipata taarifa za tukio hilo katika kituo cha Ubungo na kwenda katika
chumba cha kijana huyo kilichokuwa kimefungwa kwa ndani na kukuta mwili
wa msichana huyo ukiwa umejeruhiwa.
Alisema
baada ya kumhoji mtuhumiwa, alisema alifanya hivyo kutokana na wivu wa
kimapenzi, kwani alikuwa na uhusiano na msichana huyo lakini wazazi wa
msichana hawakutaka amwoe, hivyo kumtaarifu kuwa amepata mchumba
mwingine.
Alipoulizwa
kwa nini hakutoa taarifa katika kituo cha Polisi Kimara alikofanyia
mauaji, alisema aliogopa watu wa maeneo yale wangempiga na kumwua, kwa
kitendo hicho.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Tumbi, Kibaha, huku kijana huyo akishikiliwa na Polisi.
-Zero99
-Zero99