Meya wa jiji la Toronto nchini Canada, Rob Ford
amekiri kutumia dawa za kulevya aina ya cocaine lakini amesema
hatajiuzulu nafasi yake hiyo ya uongozi kwa kuwa ameshaomba msamana na
haya ni mawimbi tu yatapita.
Kwa miezi kadhaa Meya huyo alikuwa
akipinga habari ziliripotiwa kuhusu tuhuma za yeye kubwia dawa za
kulevya, taarifa ambazo zilionekana kufifia nguvu na pengine kufa hadi
siku ya Alhamisi ya wiki iliyopita, pale Chifu wa Polisi wa Toronto, Bill
Blair aliposema kuwa walikuwa wakifanya uchunguzi ambao asa umewawezesha
kupata video isiyo na tashwishi ikimwonesha na
kuthibitisha
kwa picha kuwa Ford ndiye mhusika aliyetajwa kwenye ripoti hizo na
matukio ya kwenye video hiyo yanalandana na ripoti zilizotolewa kwenye
mitandao mbalimbali.
Wakili wa Ford anapinga kwa kusema kuwa video husika haimwoneshi mteja wake akibwia unga.
Jumapili,
katika kipindi cha redio kwenye kituo cha 1010 ambacho kinaendeshwa na
Ford na kaka yake, Ford amemwambia Chifu wa Polisi airuhusu video hiyo
ionekane kwa umma kwa kuwa wakazi wa Toronto wana haki ya kuiona na
kuhukumu.
Video hiyo iliripotiwa kwanza
na gazeti la Star na tovuti ya Gawker ambao wao walisema walioneshwa tu
video hiyo katka nyakati tofauti na mtu aliyetaka kuwauzia ili waitumie
kwa ajili ya habari, hivyo Gawker wakakusanya fedha na kuinunua na
baadaye wakasema hawawezi kumtambulisha mtu aliyewauzia video hiyo kwa
kuwa hawana mawasiliano naye tena.
Chifu
wa Polisi, Blair yeye alisema waliipata video hiyo wakati wakichimbua
kifa cha kompyuta, yaani 'hard drive' iliyokuwa imefutwa ili kuficha
ushahidi wa dawa za kulevya.
Ford
mwenyewe hakuzungumzia kuhusu kilichomo kwenye video hiyo akidai kuwa
ilikuwa inahusika na uthibitisho wa madai ya tukio jingine ambalo kesi
yake ipo mahakamani.
Ford ameomba
msamaha kwa makosa ambayo hakuyaweka wazi. Alisema, “Mimi ni wa kwanza
kukiri, rafiki, mimi ni wa kwanza kukiri, kuwa si mkamilifu. Nimekosa…
na ninaloweza kufanya sasa ni kuomba msamaha kwa kukosea,” Ford
amekaririwa na Reuters akitamka maneno hayo redioni na takriban saa moja
baadaye akaongeza, “Nimekosea. Sijui nianzia wapi? Kwa mfano pale
Danforth, ule ulikuwa ujinga kabisa. Sikupaswa kuwa-nzwiii pale
Danforth. Kama umepanga kwenda kunywa chupa kadhaa za pombe, unapaswa
kukaa nyumbani, basi. Huendi mbele ya kadamnasi na kujifanya shujaa
mbele ya hadhara. Ninaomba msamaha kwa dhati kabisa, kwanza kwa familia
yangu, pili kwa raia na tatu kwa walipa kodi wa jiji hili kubwa. Hakika
siwezi kubadili yaliyopita, kilichobakia ni kusonga mbele na kujifunza
kutokana na makosa na ninakuhakikishieni nimejifunza”
Reuters
inasema, ikiwa unadhani kuwa sakata hili limeongoa imani ya wapiga kura
kwa Ford, utakuwa umekosea kwani kituo cha CBC kimeripoti kuwa matokeo
ya kura za haraka haraka yanaonesha kukubalika kwa Ford kumeongezeka kwa
asilimia 5 na kufikia 44%.