Munisi, ambaye alikuwa mkazi wa Mwanza, aliwapiga risasi watu watatu akiwamo mchumba wake, Christina Alfred katika Mtaa wa Bungoni Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Baada ya kumpiga risasi mchumba wake huyo na kudhania kwamba amemuua, inadaiwa kwamba Munisi aliendelea kuwamiminia risasi watu wengine na kumuua mdogo wake Christina, Alpha (22).
Katika tukio hilo, Christina na mtu anayedaiwa kuwa mchumba wake mpya, Francis Shumila wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kujeruhiwa. Mama yake Christina, Helen Alfred amelazwa katika Hospitali ya Amana baada ya kujeruhiwa pia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marieta Minangi alisema Munisi alikutwa na bastola moja, magazini mbili na yalikutwa maganda 14 ya risasi zilizotumika na risasi mbili ambazo zilikuwa hazijatumika.
Tukio hili limetokea mwezi mmoja baada ya mwandishi wa habari wa ITV, Ufoo Saro kujeruhiwa kwa risasi na mzazi mwenzake, Anthery Mushi.
Katika tukio hilo, Mushi alijiua baada ya kumuua mama mzazi wa Ufoo na inaaminika pia tukio hilo lilisababishwa na masuala ya mapenzi.
Lilivyotokea
Mashuhuda waliokuwapo katika tukio hilo walisema mauaji hayo yalitokea saa 1.15 asubuhi baada ya Munisi kufika Ilala Bungoni na kwenda katika Klabu ya Wazee iliyo jirani na eneo yalipotokea mauaji na kunywa supu kabla ya kusogea karibu na lango la nyumba anakoishi mchumba wake.
Mmoja wa majirani, Noel Gerald alisema alimuona Munisi akiwa amesimama karibu na lango la nyumbani kwa kina Christina.
Alisema baadaye waliona gari aina ya Toyota Hilux, Surf, likitoka katika lango la nyumba hiyo na mara walimuona Munisi akimwamuru dereva ashushe kioo lakini alikataa na kudai kwamba ndipo alipoamua kuwapiga risasi waliokuwamo kwenye gari hilo.
Alidai kuwa Munisi alipiga risasi nane mfululizo huku akiwa analizunguka gari hilo na kwamba alimpiga dereva ambaye baadaye alifahamika kuwa ni Shimula. Imeelezwa kuwa majeruhi huyo ni raia wa Kenya na ni rubani wa ndege.