MBUNGE wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), ameingia katika matata. Katika kujaribu kudhibiti mtoto wa shule ambaye anadai alibakwa naye na kuambukiwa virusi vya ukimwi, mbunge huyo ametoa vitisho vya kuua mtoto huyo na kujiua kama njia ya kuepuka dhahama inayoelekea kumkabili.
Siku moja baada ya gazeti la Tanzania Daima kuripoti habari za mbunge mmoja (bila
kumtaja jina), jana asubuhi Profesa Kapuya ameibuka na kumtisha
mwanafunzi huyo mwenye miaka 16 anayesoma Shule ya Sekondari Turiani
iliyoko Magomeni jijini Dar es Salaam.
Baada ya kujua kuwa mtoto huyo ndiye alitoa habari za masahibu hayo,
ambayo mbunge hakutaka yajulikane, alimpigia simu mtoto huyo, na
baadaye kutuma meseji kadhaa za vitisho.
Jana Tanzania Daima ilishuhudia baadhi ya meseji za simu zilizotumwa na Profesa Kapuya kwenda kwa mtoto huyo.
Alfajiri saa 11:21 kupitia simu yake ya mkononi yenye namba
0784993***, Profesa Kapuya alituma ujumbe ufuatao kwa mtoto huyo:
“chagueni kunisubiri tuje tuongee au mnataka kufa?”
Baadaye saa 1:07 asubuhi, alituma ujumbe mwingine kutoka simu hiyo
hiyo kwenda kwa mtoto huyo, ukisema: “Mkiuawa, itakuwa nzuri,
itawapunguzia gharama za kuishi. Usitake kugombana na serikali, mtoto
mdogo kama wewe. Sisi ndo wenye nchi yetu.
“Mwambieni Mbowe mwenye hilo gazeti awape nyumba ya kuishi. Si
mmemuingizia hela leo? Mnatumika bure watu wanaingiza hela nyingi,
mmenitibua lazima niwauwe wiki hiii haitaisha, nitapanga kambi popote.
“Jana si wamekuficha? Tuone kama utalindwa milele. Kazi ya kulindwa
imeisha, maana wameshatengeneza hela. Lazima mvae sanda. Hilo sio ombi,
ni wajibu wenu. Mnajitia mafia watoto sio? Watoto wetu wanauza unga,
nani anawakamata? Nani atapigana nasi?”
Hata hivyo, baada ya kuhisi kuwa watoto hao wamedhamiria kumchukulia
hatua, na wamewasiliana na taasisi mbalimbali za kiraia na serikali
zenye uwezo wa kumtia adabu, mbunge huyo alimtumia mtoto huyo ujumbe wa
kuonyesha alikuwa anafikiria kunywa sumu..
Ujumbe huo uliotumwa kwa mtoto huyo saa 11:2 3 ulisema: “nimewakosea
sana, acha nife mie nakunywa sumu nijiue, na nyie mje mnizike.”
Hasira za Profesa Kapuya dhidi ya mtoto hao zilitokana na hatua ya
mtoto huyo na dada yake kufichua unyama wanaodai kutendewa na mbunge
huyo, ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa za uwaziri katika Serikali
ya Awamu ya Nne.
Tangu alipogundua kuwa mtoto huyo alizungumza na gazeti hili juzi,
saa 5:17 usiku wa kuamkia jana alituma ujumbe usemao: “Si mpo Bilz?
Sasa tupo pamoja na nyie mpaka usiku.”
Baadaye saa 5:31 alituma ujumbe huu: “Hivi hamkubali kushindwa? Leo ulifuata nini ofisi ya CCM?”
Ujumbe huo ulitokana na ukweli kwamba dada wa mtoto anayedaiwa
kubakwa alifika Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi asubuhi
kuonana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, ili kuomba
chama kimsaidie kumbana Profesa Kapuya, ambaye alikuwa ameanza
kuwatisha yeye na mdogo wake.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mtoto huyo, Kinana alisema suala hilo si la chama bali la Profesa Kapuya binafsi.
Mtoto huyo alikataa ushauri wa kupeleka shauri hilo mbele ya vyombo
vya sheria, akidai kuwa jitihada zake zimekuwa zinazimwa na mbunge huyo
anayedai serikali haiwezi kumfanya lolote.
Alisisitiza kuwa hana imani na serikali, lakini akasema yupo tayari
kuchukua hatua kali dhidi ya Profesa Kapuya iwapo atasimamiwa na
watetezi wa haki za binadamu.
Baadhi ya mashirika yanayotetea makundi kadhaa yakiwamo Kituo cha
Sheria na Haki za BInadamu (LHRC) na Mtandao wa Kijinsia Tanzania
(TGNP) yalijitokeza kumsaidia watoto hao, ambao ni yatima.
Mtoto huyo na dada yake, wakizungumza na gazeti hili kwa hofu
mafichoni, walisema kwa sasa hawana imani tena kama kuna serikali
nchini Tanzania kwa kuwa wamedhalilishwa, wametembezwa hadi Bungeni na
wabunge bila hatua kuchukuliwa, licha ya kutoa taarifa katika kituo cha
polisi Oysterbay tangu mwaka jana.
Hata hivyo, kabla ya tukio la watoto hao kuripoti, ofisi za gazeti
hili juzi usiku kulikuwa na watu waliokuja wakiwatafuta watoto hao,
huku wakiwatisha kwa simu na kuwatolea maneno ya kejeli, wakidai
watawamwagia tindikali.
Mmoja wa watoto hao, alidai kuwa miongoni mwa vijana waliokuwa
wanawatisha juzi walikuwa katika gari T170 BGY, Benz, Cream Metalic,
ambayo inamilikiwa na mbaya wao.
Jana gazeti hili lilichapisha habari kuwa mwanafunzi huyo
aliyesema kuwa waziri huyo alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii
iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo hicho
katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012
alipoitwa kwenda kuchua ada kwa mara ya pili.
Akizungumza kwa uchungu, alisema mbunge huyo alifanya kitendo hicho
kwenye Hoteli ya Giraffe, Jijini Dar es Salaam mwaka 2011.
Alisema kuwa yeye alikuwa na urafiki na mwanafunzi mwenzake Zuhura
Mwaking’inda. Mwaking’inda amewahi kuwa Diwani wa Kata ya Sinza Jimbo
la Ubungo, Jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, rafiki yake (mtoto wa Mwaking’ida)
alikuwa amepooza hivyo alikuwa analazimika kumhudumia hali
iliyowaunganisha hadi huyo mtoto alipochukua jukumu la kumtambulisha
kwa baba yake ambaye naye alimtambulisha kwa Kapuya ili aweze kumsaidia
fedha kwa jili ada.
Mwanafunzi huyo alisema baada ya kutambulishwa aliitwa katika hoteli
moja jijini Dar ambapo baada ya kufika mapokezi wafanyakazi wa hoteli
hiyo walimkataza kuingia chumbani katika maana kwamba umri wake alikuwa
mdogo (mwaka 2011 alikuwa na miaka 14), lakini Kapuya aliamrisha aje
chumbani pamoja na dereva na kumwingiza kwa nguvu.
Akiwa chumbani alimlazimisha kulala naye kisha kumpa sh laki saba,
badala ya sh elfu sitini na saba kiasi ambacho kilikuwa ndio mahitaji
halisi ya ada.
Mwanafunzi huyo amesema baada ya muhula mmoja aliitwa tena na mbunge
huyo katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala tarehe 3
June 2012, ambapo pia alimlazimisha kulala naye kwenye zulia la ofisi
yake, kisha kumpa sh 350,000/.
Alisimulia kwamba wakati anatoka kwa huzuni ofisini kwa mbunge huyo,
mmoja wa wahudumu wa hapo alimuuliza kwanini anatoka kwa huzuni,
alimweleza kisa hicho, na huyo mama aliangua kilio kwa kumwambia
“mwanangu umekufa pole tu, huyu baba ni muathirika wa ukimwi”.
Aliongeza kuwa baada ya kuambiwa vile alilia na kufanya fujo hapo
mapokezi hadi alipokamatwa na walinzi wa kisha kupelekwa kituo cha
polisi kufunguliwa mashtaka, lakini akiwa polisi alipoeleza mkasa wote,
Polisi walilazimika kumwita Kapuya na wakawasuluhisha kwa makubaliano
kwamba Kapuya atakuwa anamlipia ada, na kumpa pesa za matumizi sh. laki
tatu kila mwezi, jambo ambalo amekuwa akilitekeleza kupitia simu yake
ya mkononi 0755993***.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, 24 Januari 2013, alifika mtu
nyumbani kwao mtu mmoja (jina tunalihifadhi) na kujitambulisha kuwa
yeye ni jambazi na kuwa alitumwa kwenda kuwaua kwa malipo ya sh.
milioni 50, lakini alipokuta ni watoto wadogo aliwasamehe, na kusema
yeye ni jambazi sugu hawezi kupoteza nguvu zake kuua vitoto.
Alienda akiwa na bastola, maji kwenye chupa yanayodhaniwa kuwa ni
tindikali na bomba la sindano. Kwa mujibu wa mtoto huyo, jambazi huyo
anasema kuwa tayari alilipwa milioni 15 za awali.
Mtoto huyo alisema jambazi huyo aliwambia kuwa yeye ni rafiki wa
mtoto wa Kapuya na wanamfahamu vizuri, lakini hataweza kuaua baada ya
kubaini kuwa wao ni yatima tu.
Hata hivyo kufikia mwezi Februari mwaka huu, mtu asiyefahamika
alienda nyumbani na kutelekeza gari aina ya T.199 BGY Mercedes Benzi ya
Blue wakati wanafunzi hao wakiwa shuleni, kisha kuacha ufunguo kwa
jirani yao kwa maelekezo kuwa wakifika awapatie.
Na Kapuya aliwapigia simu kuwaarifu kuwa amempa zawadi ya gari kwa
ajili ya matumizi ila yeye na dada yake wanaruhusiwa kuuza ili wapate
pesa kwa ajili ya mahitaji yake siku zilizosalia, kwani muda sio mrefu
baada ya uchguzi mkuu 2015, Kapuya atakuwa Waziri Mkuu, hivyo itakuwa
ngumu yeye kumtumia huyo binti pesa kama alivyoelekezwa na jeshi la
polisi kituo cha Oysterbay.
Baada ya mwanafunzi huyo na dada yake ambaye ana umri wa miaka 20,
kupewa gari walishindwa kulitumia hivyo kutoa taarifa polisi kwani kwa
kupokea gari hilo ilikuwa ni kuwatelekeza kwani yeye hana hata hela ya
kuweka mafuta ya gari, hivyo walienda polisi ili kesi ipelekwe
mahakamani kumshtaki kapuya.
Polisi wa Oysterbay walikubali kulipeleka tatizo hilo kwa Katibu wa
Bunge, ambaye alimwita mwanafunzi huyo na mdogo wake waende Dodoma
kukutana na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ingawa
walipofika Dodoma walikaa na kamati ya hiyo kwa maelezo kuwa Kapuya
hakuwepo hadi Bunge lilipoisha walirejeshwa Dar es Salaam.
Mtoto huyo na dada yake alitoka ofisi za CCM lakini akiwa anaelekea
kituo cha basi alithadharishwa na mwanafunzi mwingine kwa haraka kuwa
akimbie kwa kuwa atamwagiwa tindikali na watu waliokuwa wanamfuata
nyuma, alikimbilia katika mtaa wa Hoteli ya Star light kisha aliomba
msaada baada ya kupotea njia na hivyo alisaidiwa na mama mmoja
kufikishwa chumba cha habari cha Channel Ten.
Ni katika chumba hicho ndio mwandishi wa habari hizi alienda na
kuwakuta watu wawili hao waliokuwa wanamhitaji binti huyo lakini
walikatazwa kumchukua.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima