WATU wanne wamekufa katika matukio manne tofauti jijini Dar es Salaam, likiwemo la kukutwa maiti ya mtoto mchanga wa kike anayekadiriwa kuwa na umri wa siku moja.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke Engelbert Kiondo, maiti ya mtoto huyo iliokotwa juzi saa 6:00 mchana katika maeneo ya Mtoni Relini Dampo, ambapo ilikutwa imewekwa ndani ya mfuko wa plastiki na kutupwa katika eneo hilo na mtu asiyefahamika.
Maiti imehifadhiwa katika hospitali ya Temeke na upelelezi unaendelea. Kamamda Kiondo alisema katika tukio jingine, watu wawili wamekufa katika maeneo ya Mbande na Chamazi huku chanzo cha vifo vyao kikiwa hakijajulikana.
Alisema mkazi wa Mbande, Rashid Meso (26) akiwa katika biashara zake eneo la Mbande alianguka ghafla na kufa akiwa njiani kupelekwa hospitali ya Temeke.
Mtu mwingine Juma Kasongo ambaye ni mchungaji wa ng'ombe wanaomilikiwa na Donald Michael (39) ambaye alikutwa akiwa kitandani kwake akiwa ameshakufa huku akitokwa na povu mdomoni.
Maiti zimehifadhiwa katika hospitali ya Temeke kwa uchunguzi zaidi na upelelezi unaendelea. Katika tukio jingine, Dia Haruna (6) amekufa baada ya kugongwa na gari akivuka barabara katika eneo la Majohe, Wilaya ya Ilala.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema gari aina ya Toyota Avensis yenye namba T 636 BYL ikiendeshwa na Njile Mlacha (39) mkazi wa Majohe, akitoka kwa Diwani kwenda Kwa Mpogo alimgonga mtoto huyo na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
Majeruhi alikufa muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya Amana, maiti imehifadhiwa hospitalini hapo na dereva wa gari hilo amekamatwa.