Akifunguka kikamilifu kuhusiana na ‘saga’ hilo, kwa sauti imara bila wasiwasi, Kapuya alisema kuwa anamjua mwanafunzi husika, kisha akasema:
“Kuna watu wanamtumia. Hili suala limetengenezwa ili kuniharibia malengo yangu.”
ACHAMBUA UTAPELI WA MWANAFUNZI
KESI A; Mwanafunzi aliyedai kubakwa, alinukuliwa mitandaoni akisema kuwa yeye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Turiani, Magomeni, Dar es Salaam.
Kapuya anapangua: “Huyo muongo, alinifuata kuniomba ada ya chuo. Aliniambia anasoma Chuo Kikuu cha Tumaini.”
KESI B; Mwanafunzi huyo alisema anasoma kidato cha tatu na alibakwa mara mbili na mheshimiwa huyo.
Kapuya anajibu: “Achilia mbali yeye, mimi sijawahi kubaka katika maisha yangu yote. Kuhusu kidato cha tatu, yeye mwenyewe aliniambia anasoma Tumaini University na aliomba nimlipie ada ya miaka miwili ambayo ni shilingi 3,000,000.
“Kwa mara ya kwanza nilimpa shilingi 2,300,000 na baadaye nilimpa shilingi 700,000. Kipindi hicho nilikuwa sijagundua kama ni tapeli, ila baadaye nilipogundua utapeli wake, nilihakikisha hanisogelei. Hapa nawajua watu wengi aliowatapeli.”
Kuthibitisha anachokisema, Kapuya alitaja jina la mkurugenzi wa benki moja nchini (jina tunalihifadhi) kuwa alishalizwa na mwanafunzi huyo.
KESI C; Denti huyo alidai ana umri wa miaka 16.
Hilo nalo Kapuya analipangua hivi: “Hata mimi mwanzoni aliponifuata nilijua ni binti mdogo, yatima anayehitaji msaada lakini ukweli ni kwamba yule ni mama mzima na ana mtoto. Ameshazaa yule.
“Hasomi popote, Mungu amemsaidia kuwa na umbile dogo ambalo analitumia kuwatapeli watu kwamba ana umri wa miaka 16, ni tapeli mkubwa, tena wa kuogopwa kabisa.”
KESI D; Mwanafunzi mwenyewe alidai kuambukizwa Ukimwi na kiongozi huyo aliyewahi kuongoza wizara mbalimbali nchini.
Kuhusu hilo, Kapuya alicheka kidogo halafu akajibu: “Sina Ukimwi, afya yangu ipo imara sana. Kama yeye ana Ukimwi, basi aseme mahali alipoutoa, siyo kusema uongo na kutaka kunichafua mbele ya jamii ambayo inaniheshimu.”
KESI E; Denti amedai kutumiwa SMS za vitisho kwamba mheshimiwa huyo amedai atamuua.
Hivi ndivyo Kapuya anavyojibu: “Sijawahi kutuma SMS za vitisho. Unajua haya mambo nashangaa sana, nipo huku kijijini Kaliua, kwa hiyo mambo mengi nafanya kuambiwa kwa sababu sipati magazeti kwa wakati.
“Nina laini tatu, Tigo, Airtel na Vodacom, hata siku moja sijawahi kutuma SMS ya kumtishia mtu kumuua. Hao wanaomuamini, waendelee kumuamini huyo tapeli lakini lazima nimfikishe kwenye vyombo vya sheria.”
KESI F; Yapo madai kuwa Kapuya alitishia kujiua baada ya kugundua ameshikwa pabaya na denti huyo.
Hilo nalo Kapuya alilijibu hivi: “Nimesema sijatuma SMS yoyote, wala siwezi kutishia kujiua. Nitishie kujiua kwa lipi?”
KESI H; Miongoni mwa madai yaliyotajwa ni kwamba Kapuya anajindaa kuwa waziri mkuu baada ya Uchaguzi Mkuu 2015.
Kuhusu hili, Kapuya alicheka akasema: “Nilimwalika Lowassa (Edward) jimboni kwangu. Akiwa huku na maeneo mengine ya Mkoa wa Tabora, wananchi walisema mimi ndiye nitakuwa waziri mkuu wake.
“Yalikuwa ni maneno tu na mimi nilianza kuyasikia kipindi hicho. Kwa hiyo sijawahi kutamka popote kuwa mimi najiandaa kuwa waziri mkuu.”
MTAZAMO WAKE
Pamoja na kupangua madai yote hayo, Kapuya aliongeza kuwa yapo makundi mawili ambayo anayahisi kuwa ndiyo yapo nyuma ya denti huyo ambaye yeye amemwita ni mama mtu mzima.
Alisema: “Kuna majambazi fulani alikuwa anawatumia kunishawishi niwape pesa, baadaye waligombana. Wale majambazi walimwambia watamuua ikiwa yeye ataniendekeza.
“Nahisi hao ndiyo yupo nao kundi moja kuhakikisha wananichafua baada ya mimi kugundua uhuni wao ambao walikuwa wananifanyia. Nitakapoanza kuwashughulikia kisheria, itajulikana tu nani na nani anahusika nyuma yake.”
Aidha, Kapuya alimtaja mwanasiasa mmoja mwandamizi nchini (jina tunalo), mwenye asili ya Mkoa wa Tabora, mwanachama wa CCM kuwa anamhisi yupo ndani ya mkakati huo wa kumchafua.
“Ni hivi, … (anataja jina la mwanasiasa huyo), ameshapandikiza vijana wawili ili waniangushe kwenye Uchaguzi Mkuu 2015. Hao vijana wametengeneza tovuti ambayo imekuwa ikinichafua sana.”
MADAI YA MSINGI
Mwanafunzi huyo ambaye Kapuya amemwita ni mama mwenye mtoto, aliripotiwa na mitandao mbalimbali ya kijamii akidai kubakwa kisha kuambukizwa Ukimwi na kiongozi huyo.
Katika madai yake, mwanafunzi huyo alisema kwamba zahama hiyo ilimpata baada ya kwenda kwa Kapuya kuomba msaada wa ada ya shule ndipo kiongozi huyo alimgeuzia kibao.
chanzo:globalpublishers