MBALI na mtu mmoja kufariki dunia na wengine 24 kujeruhiwa na kulazwa
kwenye Hospitali ya Bwagala, Turiani mkoani hapa, mwanaume mmoja
amekatwa nyeti zake katika mapigano ya wakulima na wafugaji Jumanne
iliyopita.
Mapigano
hayo yaliyoshuhudiwa na mwandishi wetu yalipoteza amani iliyokuwa
kwenye Kijiji cha Dihombo Kata ya Hembeti Wilaya ya Mvomero.
Mashuhuda kadhaa walimwambia mwandishi wetu kwamba, mtu aliyekatwa
nyeti alikutana na wakulima hao wenye hasira waliokuwa wakimvamia mgeni
yeyote waliyemuona mbele yao.“Wakulima walikuwa na silaha za jadi kama vile mapanga, mishale ya sumu na marungu, walimkuta mtu huyo aliyekuwa akipita na kumvamia kisha kumpiga na alipoanguka chini mkulima mmoja alimkata nyeti zake,” alisema shuhuda aliyejitambilisha kwa jina la Kibwana.
Mtu aliyekatwa nyeti (angalia picha ukurasa wa mbele) hakufahamika jina lake mara moja, lakini baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo walisema kwamba alikimbizwa hospitali ili kunusuru maisha yake.
Hata hivyo, baadhi ya wakulima nao waliumizwa vibaya katika tukio hilo lililosababisha kifo cha mfugaji Yusuf Mdutu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile amethibitisha kutokea kwa mapigano hayo huku akisema kuwa msako mkali unaendelea kuwakamata wahusika.