Like Us On Facebook

WAPINZANI WATANGAZA HALI YA HATARI TAREHE 10 MWEZI HUU DHIDI YA SERIKALI ILIYOKO MADARAKANI



                 MUUNGANO wa vyama vitatu vya upinzani umesema kuanzia sasa haupo tayari kubatilisha kusudio lao la kufanya maandamano nchi nzima kwa kukutana na kiongozi yeyote isipokuwa tu Rais Jakaya Kikwete atapotangaza kutosaini muswada uliopitishwa bungeni kinyemela. Pia umesema hautakubali kamwe kuzuiwa na chombo chochote kufanya maandamano na mikutano ifikapo Oktoba 10 mwaka huu.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Viongozi wa Kamati ya Ufundi ya Muungano wa vyama vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.

Hao ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, Mkuu wa Idara na Taasisi za Dola na Vyombo vya Uwakilishi NCCR Mageuzi, Faustine Sungura na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Haki za Binadamu na Uhusiano wa Umma kutoka CUF, Abdul Kambaya.

Mnyika alisema uamuzi huo umefikiwa kwa pamoja na wenyeviti wa vyama hivyo vitatu kwamba muda uliobaki sasa hadi kufikia Oktoba 10 mwaka huu ni wa kukutana na makundi maalumu kuwaeleza kasoro zilizopo kwenye mswada na kuwashawishi kuwaunga mkono.

“Tunapenda kuwaeleza vyama vitatu tayari vimekamilisha maandalizi ya kufanya mikutano nchi nzima, tumejipanga kupinga Rais Kikwete kusaini muswada huo kwa njia mbalimbali zikiwamo za demekrasia, maandamano na raia.

“Jambo hili ni kubwa na lina maslahi kwa kila Mtanzania, hivyo tunaomba kila kundi na taasisi ziungana na sisi na kufanya maandamano kwa njia ile watakayoona inafaa na hata kufanya mgomo.

“Viongozi wa dini wanaweza kuandaa sala ya kuliombea taifa kupinga Rais Kikwete kutosaini muswada huo, hivyo hivyo katika taasisi nyingine kulingana na nafasi zao, nasema siku hiyo itakuwa ni ya kupinga kila kitu.

Kama ikitokea kundi linazuia mikutano hiyo au maandamano hayo kwa kusema tii sheria bila shuruti, kamwe mtu asikubali kuzuiwa, yaani tunataka siku hiyo iwe ya kupinga kila jambo litakalijitokeza kwa lengo la kukwamisha,”alisema.

Abdul Kambaya kutoka CUF, alisisitiza kumuomba Rais Kikwete kutosaini muswada huo na badala yake kuurudisha bungeni kuufanyia marekebisho ambayo yanalalamikiwa


-Mtanzania
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari