WACHEZAJI wa Yanga wameibua kitu ambacho hauwezi kukitarajia. Kumbe huwa hawafanyi mazoezi ya kupiga pasi na chenga tu, bali pia hufanya mazoezi ya bendi kwa ajili ya kushangilia mabao wanayofunga.
Kama ni mtazamaji mzuri wa mechi za soka za Ligi
Kuu Bara inayoendelea, utakuwa umegundua staili mpya ya ushangiliaji wa
mabao ya wachezaji hao ambayo kumbe ina jina lake kabisa.
Wachezaji ambao mara kwa mara wamekuwa wakijumuika
kwenye shoo hiyo ni Didier Kavumbagu, Jerry Tegete, Hamisi Kiiza, Simon
Msuva, David Luhende na Mbuyu Twite.
Mwanaspoti ilimuuliza Msuva naye alisema: “Kwa
bahati nzuri mimi ndiye kiongozi wa shoo nzima na ndiye niliyebuni aina
hii ya ushangiliaji wa mabao.
“Kimsingi ni kwamba kabla ya mechi huwa tunakutana
na kuchagua wimbo mmoja na kuufanyia mazoezi, lakini ni kwa yule
anayetaka tu, hatumlazimishi mtu. Tutakuwa tunafanya hivi kila mechi
tutakayobahatika kufunga mabao,”alisema Msuva ambaye aliwahi kuwa dansa
wa kikundi cha vipaji cha Tanzania House of Talent (THT).
Kiiza yeye alienda mbali baada ya kusema kundi
hilo linajulikana kwa jina la ‘Danger Zone Band’ (DZB). Staili yao
ambayo imekuwa kivutio kwa mashabiki ni ya baadhi ya wachezaji wa timu
hiyo kujipanga mstari mmoja na kucheza mojawapo ya nyimbo za wanamuziki
wa Bongo Flava hasa Diamond.
Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba, wote
wamekuwa wakicheza staili moja pasipo mwingine kwenda tofauti na
wenzake, hivyo kufanya ionekane kama bendi rasmi ya muziki.
Hayo ndiyo mambo ya Yanga bwana!
-mwanaspoti
-mwanaspoti