Msemaji huyo amemkariri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon akilaani vikali mauaji hayo yaliyotokea wakati waasi wa M23 waliposhambulia walinda amani hao wa MONUSCO ambao walikuwa wakisaidia jeshi la DR Congo, FARDC kulinda raia huko Kiwanja-Rutshruru, kilometa 25 kaskazini mwa Goma.
Ban ametuma rambirambi kwa familia ya askari huyo pamoja na serikali ya Tanzania huku akisema kuwa Umoja wa Mataifa umejizatiti kuchuka hatua zote muhimu kwa mujibu wa azimio namba 2098 la Baraza la usalama kuhusu kulinda raia Mashariki mwa DR Congo.
Wakati huo huo, jeshi la DR Congo limewaambia waandishi wa habari kwamba ilikomboa miji miwili mingine ya Rutshuru na Kiwanja, katika jimbo la Kivu kaskazini kutoka kwa wapiganaji wa M23 karibu na mpaka wa Rwanda.
Jana yake, yaani Jumamosi, jeshi hilo liliripoti kuteka mji wa Kibumba ulioko kilometa 20 kutoka Goma Kaskazini. Mapigano yalizuka Ijumaa, siku chache baada ya mazungumzo ya amani ya mjini Kampala, Uganda, kuvunjika..
Kanali Olivier Hamuli msemaji wa jeshi la DR Congo ameeleza kuwa,jeshi hilo limesema kuwa limepata mafanikio makubwa zaidi dhidi ya waasi wa M23 katika siku ya pili ya mapigano makali na kwamba waasi hao wamerejea nyuma kwa kukimbilia katika milima ya karibu na mpaka wa Rwanda, kutoka mashariki mwa nchi hiyo.
Jeshi la Kongo pia limeitaka nchi jirani ya Rwanda kuisaidia Kinshasa kupokonywa silaha waasi hao.
Bertrand Bisimwa kiongozi wa kisiasa wa kundi la M23 amethibitisha kwamba mapigano hayo yanaendelea na kwamba sasa yameelekezwa upande wa Kaskazini. Ijumaa waasi wa M23 walidai kuwa jeshi limeshambulia kambi zao, lakini jeshi lilisisitiza kuwa lilishambuliwa kwanza madai ambayo yanaungwa mkono pia na duru za MUNOSCO.
SOURCE: WAVUTI