Like Us On Facebook

VYOMBO VYA HABARI VIKINYAMAZISHWA MAWE YATAPIGA KELELE..

WIKI iliyopita, tasnia ya habari na Watanzania walipatwa na mshtuko baada ya serikali kuamua kuyafungia magazeti ya kila siku ya Mwananchi na Mtanzania. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gazeti la Mwananchi limefungiwa kwa siku 14, na Mtanzania siku 90 sawa na miezi mitatu. Mfukunyuku nimelazimika kulifukua hili ambalo linakumbusha kidonda au kovu lisilopona baada ya ubabe huo kutumika na kulipeleka kifungo kisicho na ukomo gazeti la Mwanahalisi ambalo sasa limetimiza mwaka mmoja na miezi kadhaa tangu kufungiwa. Ni hukumu mbaya ambayo haipaswi kujadiliwa kutokana na ukweli kuwa kifungo chochote ni lazima kiwe na ukomo. Pamoja na kuwa ubabe huo umepigiwa kelele na makundi mengi yakilaumu hatua iliyochukuliwa na serikali dhidi ya vyombo vya habari vinavyoonekana kuwa mwiba kwa upande wake, lakini hilo haliwezi kufanikisha kamwe Watanzania kukosa habari. Sheria mbovu na ulevi wa madaraka vinaweza kuwa chanzo cha vyombo vingi vya habari kuchukuliwa hatua, iwapo hatutakuwa tayari kupinga jambo hilo. Ingawa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewasilisha kwa Katibu wa Bunge muswada binafsi bungeni ili kufuta sheria ya magazeti ya mwaka 1976 bado harakati zinahitajika katika hilo. Sheria hiyo inampa madaraka Waziri wa Habari kuamua anapojisikia kufungia chombo chochote huku yeye akiwa ndiye mahakama na hakimu. Ni sheria mbovu isiyofaa hata kusomwa mbele za watu. Serikali inakosea na inapokosea ni lazima ielezwe. Katiba tunayojaribu kuitengeneza upya inasema wazi kuwa kuna uhuru wa kutoa maoni. Ni uhuru upi huo tunaouzungumza ikiwa kuna kuminya uhuru wa habari? Halafu serikali inapokuja na hoja ya kusema uchochezi juu ya habari zinazoandikwa mbona kuna chombo cha habari kilichowahi kutoa takwimu za kuonyesha idadi ya Wakristo na Waislamu, tena kwa kukopi takwimu za mtandaoni? Je, huo sio uchochezi? Mbona haikuwahi kushughulika na chombo hicho au kwa vile inakimiliki? Kuna methali moja inasema kuwa ukiona mwenzako ananyolewa wewe tia maji, ni lazima vyombo vya habari vitafakari kwa kina uonevu huo unaofanywa na serikali dhidi ya tasnia hiyo. Kama hatutakuwa na umoja na baadhi kuchekelea lile linalowakuta wengine ni wazi tutakuwa tunajidanganya. Leo vyombo vya serikali kama vitakuwa vinachekelea hayo, kuna wakati utafika navyo vinaweza kujikuta muhanga wa uonevu huu. Ndiyo, kuna mabadiliko yanayoweza kutokea katika taifa, kuna kuanguka kwa serikali hatua inayoweza kupelekea vyombo hivyo vikachomwa na mwiba huo huo unaochoma vyombo ambavyo sio vya serikali. Ndiyo maana nasisitiza kuwa hakuna shangwe katika jambo hilo, ni lazima tukae kwa umoja na kutafakari wapi tunapohitaji kuelekea. Kama tupo tayari kuendelea kuonewa na udhalimu huu huku wengine wakiumia, nayo inahitaji tafakari. Lakini nikumbushe tukio la kuhuzunisha, la kinyama lililotokea mwaka mmoja uliopita ambapo Jeshi la Polisi linahusishwa na mauaji ya mwanahabari mwenzetu wakati akiwa kazini. Unafikiri tukio lile lilistahili kumpata Daudi Mwangosi? La asha. Linaweza kumkuta yeyote yule aliyeko katika tasnia hii, haijalishi ni wa chombo cha serikali au cha mtu binafsi. Ndiyo maana hata katika tukio hilo la kusikitisha baadhi walitolea wito kwa wanahabari ‘kulisusia’ Jeshi la Polisi ambalo lilihusishwa na mauaji ya mwandishi huyo. Lakini baadhi ya wanahabari walipuuzia wito huo ambao ulipaswa kufikisha ujumbe muhimu kwa jeshi hilo kuhusu haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari. Ukitafakari kwa kina hakuna hoja ya msingi unayoweza kuiona katika kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, ni utashi binafsi wa wasimamizi wa serikali uliowaongoza na wala sio madhara ya uchochezi kama unavyozungumzwa katika taarifa hizo. Kama kweli serikali ina nia thabiti ya kutaka kuhakikisha inaandikwa kwa mazuri, basi inapaswa pia kusimamia vyombo vyake vya dola katika kutoa haki. Haiingii akilini hata kidogo kuwa waumini wamezoea kusali bila kusimamiwa, leo wanawekewa ulinzi na chombo cha habari kinapokwenda kuandika hivyo, unalalamika na kusema uchochezi. Hivi unaweza kumtenganisha polisi na kuwa na mbwa anapofanya ulinzi? Hapana ni serikali kuamua. Mfukunyuku anaamini kuwa tatizo serikali haitaki kukubali kuwa imeshindwa katika maeneo mbalimbali. Huwezi kusema eti waraka wa mishahara iliyotolewa na chombo cha habari ni wa siri wakati taarifa hiyo ilishawahi kutolewa na Rais Jakaya Kikwete katika sherehe za wafanyakazi juu ya kuongeza mishahara. Nilitegemea serikali ilalamikie taarifa kuwa sio ya kweli, labda imepotoshwa na sio huo waraka kuwa wa siri. Kabla ya kuanza kushughulikia chombo cha habari wangelazimika kumtafuta mchawi aliyevujisha huo waraka. Hilo lingekuwa la maana. Lakini kitendo cha kufungia vyombo vya habari ni kutaka kuwanyima Watanzania fursa ya kupata habari. Ni vema serikali ikatambua kuwa kukataa kusikia ukweli hakuufanyi ukweli huo kuwa uongo. Vyombo vya habari walivyovifungia vimekuwa na mchango mkubwa kwa serikali, na vimekuwa vikitoa taarifa za muhimu juu ya yanayoendelea ndani na nje ya nchi hii. Mfukunyuku anaamini kuwa kitendo cha kuminya vyombo vya habari na kushindwa kusainiwa kwa sheria ya vyombo vya habari iliyotungwa na Bunge ni kuendeleza udhalimu wa kutaka masuala yaliyo na muhimu kushindwa kuripotiwa na hata kutolewa kwa umma wa Watanzania. Tena kuna kesi iliyofunguliwa juu ya kupinga sheria hiyo kutoanza kusikilizwa mahakamani kwa miaka minne sasa kutokana na kutopangiwa jaji wa kuisikiliza. Hivi leo ukiandika juu ya jambo hilo utaonekana kuwa mchochezi wakati ni kitu cha kweli cha haki kushindwa kutendeka? Tusijidanganye hata kidogo kuwa tukiminya vyombo vya habari ndiyo madudu yanayofanywa na watu wasio waaminifu yatashindwa kuandikwa. Hata kama wameamua kuingia hadi katika mitandao ya kijaami, bado masuala ya wizi wa fedha za nje (EPA), kutoroshwa kwa wanyama wetu, mabilioni yaliyoibwa kwa Watanzania yanazidi kutunisha akaunti za mafisadi huko Uswisi, nchi yetu kuwa uchochoro wa kupitisha na kuingiza dawa za kulevya vitaibuliwa tu. Nimalizie kwa kusema kuwa juhudi zozote za kuvinyamazisha vyombo vya habari havitalisadia taifa hili na wala hazitafanikiwa kwa sababu kama wanachokieleza ni ukweli, hata kama wakinyamaza wao, basi mawe yatapiga kelele. Makala hii imeandikwa na Betty Kangonga Source: Tanzania Daima Jumapili
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari