NYOTA aliyesajiliwa kwa gharama kubwa msimu huu
katika kikosi cha Arsenal ni Mesut Ozil. Nyota huyu tayari
amethibitisha ubora wake kwa kuonyesha uwezo wa kujitambua, kutuliza na
kutoa pasi sahihi, pia ana uwezo wa kucheza kitimu.
Ozil ambaye ni raia wa Ujerumani mwenye asili ya
Uturuki alisajiliwa na Arsenal msimu huu kwa Pauni 42.5 milioni akitokea
klabu ya Real Madrid na kusaini mkataba wa kuitumikia Arsenal kwa miaka
mitano.
Baada ya kusaini mkataba huo, Ozil alipohojiwa na
vyombo vya habari alisema: “Ni kweli nilitaka kubaki Real Madrid, lakini
baadaye niligundua kwamba kocha au benchi la ufundi halina imani na
mimi. Mimi ni mchezaji ninayependa kuaminika, ndiyo maana nimehama
Madrid na kujiunga na Arsenal ambayo inaonyesha itaniamini.”
Hata hivyo, wachezaji wengi wa Real Madrid
hawakufurahishwa na uamuzi wa Ozil kuhama Real Madrid, miongoni mwao
alikuwa ni nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ambaye alisema:
“Alikuwa ni mchezaji anayejua kwa kiwango cha juu kunichezesha tukiwa
tunashambulia, nimekasirika kwa kuondoka Ozil.”
Kutuliza na kutoa pasi sahihi
Ozil aliichezea Arsenal kwa mara ya kwanza
Septemba 14, 2013 katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Sunderland
ugenini, katika mechi hiyo alimpa pasi nzuri Olivier Giroud aliyeitumia
vizuri kuipatia Arsenal bao dakika ya 11. Mechi hiyo ilimalizika kwa
Arsenal kushinda 3-1 ikiwa ni mechi ya nne msimu huu wa ligi.
Siku tatu baadaye, Ozil aliichezea Arsenal kwa
mara ya kwanza katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya
Marseille, ambapo Arsenal iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini
ambayo yalifungwa na Theo Walcott na Aaron Ramsey.
Ozil aliichezea Arsenal mechi yake ya kwanza ikiwa
nyumbani wakati walipocheza na Stoke City Septemba 22 na Arsenal
kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 huku mabao ya Arsenal yakifungwa na
Aaron Ramsey, Per Mertesacker na Bacary Sagna.
Pia Septemba 28, Arsenal ilicheza dhidi ya Swansea na kushinda 2-1 hivyo kukaa kileleni mwa Ligi Kuu England.
Katika mechi zote hizo Ozil alifanya vizuri katika kutuliza mpira na kutoa pasi sahihi.
Oktoba 2, Ozil alidhihirisha ubora wake baada ya
kuiongoza Arsenal kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Napoli katika
mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Katika mechi hiyo alifunga bao la
kwanza katika dakika ya nane na baadaye alitoa pasi kwa Olivier Giroud
aliyeipatia Arsenal bao la pili katika dakika ya 15.
Si mbinafsi
Ozil ni kiungo mshambuliaji anayejionyesha kwa jinsi
anavyocheza, haijifichi, ana kipaji cha juu ingawa ni hatari kuwa na
mchezaji maarufu katika sehemu inayohitaji ubunifu ambayo ni kiungo
mshambuliaji au mchezeshaji wa timu. Kama mchezaji anayecheza sehemu
hiyo ya kiungo ni mbinafsi, basi atashindwa kutekeleza wajibu wake wa
kuiendesha timu. Lakini Ozil yupo tofauti, yeye anacheza kitimu zaidi,
ana uwezo wa kuwadanganya wachezaji wa timu pinzani na hivyo kuwapa
nafasi washambuliaji kuwa huru na kuwapasia wakiwa katika sehemu nzuri
ya kufunga. Ozil alifanya hivyo alipokuwa Real Madrid, alikuwa akimpa
pasi nzuri za kufunga Cristiano Ronaldo na anafanya hivyo kwa Giroud
katika Arsenal.
“Wachezaji wenzangu wananijua mimi ni mchezaji ambaye si mbinafsi,” alisema Ozil alipojiunga na Arsenal.
Fundi wa mipira ya adhabu
Ozil ni fundi wa kupiga mipira ya adhabu.
Anatarajiwa ataisaidia sana Arsenal katika kupiga mipira ya adhabu
ambayo italeta mabao. Katika mechi ya Ligi Kuu waliyocheza dhidi ya
Stoke City Septemba 22 na Arsenal kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, mabao
yote ya Arsenal yalipatikana kutokana na mipira ya adhabu iliyopigwa na
Ozil.
Mchezaji asiyetumia nguvu nyingi
Upo msemo usemao kuwa mashabiki wa soka wa England
wanapenda kuona wachezaji wanaojituma, wanaotumia nguvu, wachezaji
wanaokimbiza mpira muda wote uwanjani, lakini katika miaka ya hivi
karibuni wameibuka pia mashabiki wanaopenda wachezaji wanaocheza
taratibu bila kutumia nguvu nyingi, wanajituma na kutumia akili nyingi
uwanjani kama Dimitar Berbatov. Uchezaji huo wa taratibu bila kutumia
nguvu nyingi, kujituma na kutumia akili nyingi uwanjani, mwenyewe ni
Mesut Ozil.
-mwanaspoti