Abiria
hamsini na moja waliokuwa wakisafiri na basi la Taqwa kutoka Bujumbura
kuelekea Dar-es-Salaam wametekwa katika kijiji cha Milade wilayani
Mkalama na kuporwa mali , simu na fedha zaidi ya shilingi milioni mia
mbili hamsini.
Kwa
upande wake dereva la basi hilo bwana Ahamed Seif amesema gafla aliona
majani barabarani na alipoangalia vizuri aliona kuna mawe makubwa
mawili yakiwa barabarani na kushindwa kuyakwepa ,baada ya kugonga mawe
hayo magurudumu yote mawili ya mbele yalipasuka na gari ikaserereka
umbali wa mita mia moja.
Kwa
upande wao abiria na majeruhi wamesema waliona gari likipoteza mwelekeo
na baadaye walisikia sauti za watu zikiwaambia washuke na watoe fedha
na simu zao,lakini abiria wengine wametupia lawama kwa wafanyakazi wa
basi hilo kuchukuwa abiria wa njiani wakati basi likiwa limejaa na
abiria hao inasadikiwa ndio waliokuwa wakiwasiliana mara kwa mara na
watekaji.
Naye
mganga wa wodi ya majeruhi ya hospitali ya mkoa wa Singida Dkt Banuba
Deogratias amesema walipokea majeruhi kumi na tisa walikuwa na mipasuko
na majeraa ya kupigwa na fimbo, wameweza kuwatibu na kuruhusiwa isipo
kuwa wengi wao hawana fedha kwa sababu ni raia kutoka nchi za Burundi
na Kongo walikuwa wakisubiri kukabidhiwa kwa idara ya ustawi wa jamii
ili wasaidiwe nauli za kurudi makwao.