Hata hivyo, pamoja na umuhimu wa choo, lakini si kila nyumba iliyo na choo au hata zile ambazo zina huduma hiyo, basi vyoo ni vibovu, havina hadhi. Zipo aina mbalimbali za vyoo kwa matumizi ya binadamu katika maisha yake ya kawaida.
Vyoo vina matumizi mengi ingawa bado watu wengi hasa katika nchi maskini na zinazoendelea ikiwamo Tanzania wanatumia choo cha kuchuchumaa wakati wa kujisaidia, lakini mijini na katika nchi zilizoendelea, wao hutumia vyoo vya kukaa.
Nyumba nyingi mijini na ofisi mbalimbali zinazojengwa hivi sasa, huwekewa vyoo vya kukaa. Hata zile za zamani zinakarabatiwa na kubadilishwa kwa kuwekewa hivi ambavyo vinaonekana vya ‘kisasa’.
Mgunduzi wa vyoo vya aina hii, Thomas Crapper anasema kwa mtazamo wake aliona kukaa wakati wa kujisaidia ni utambulisho wa ustaarabu na maendeleo.
Hata hivyo, madaktari wanapingana naye wakisema kujisaidia katika vyoo vya kukaa kuna madhara kiafya kwa kuwa mkao huo unaweza kuleta matokeo mbalimbali ndani ya mwili.
Utafiti uliofanywa na mtandao wa ‘naturesplatform’ umegundua kuwa matumizi ya choo cha kukaa huweza kusababisha matatizo mbalimbali ikiwemo kansa ya utumbo mkubwa.
Mtaalamu wetu wa afya wa gazeti la MWANANCHI, Samwel Shita anasema, madhara ya vyoo vya kukaa ni makubwa kwani wakati mwingine yanaweza kuwa chanzo cha saratani ya utumbo mkubwa kutokana na haja kubwa kubaki kwa muda mrefu katika utumbo huo.
Shita anasema mtu anapojisaidia haja kubwa katika choo cha kuchuchumaa, kinasaidia haja yote kutoka kwa sababu ya msukumo unaosababishwa na mkao huo.
“Unapokaa unakuwa umekaa katika choo mwili unakuwa umelegea, hivyo inabidi utumie nguvu kubwa kujikamua kutoa haja, tofauti na unapochuchumaa,” anasema Shita na kuongeza:
“Matatizo huanza hapo, unapojisaidia ukiwa umekaa na kulazimisha kujikamua unaweza kusababisha vimishipa vidogo katika utumbo mpana sehemu ya haja kubwa ya ndani na ya nje kuvimba na maumivu makali husababishwa na ugonjwa unaojulikana kama ‘hemorrhoid,” anasema.
Anasema ‘hemorrhoid’ ni ugonjwa ambao pia huitwa bawasiri. Mgonjwa hupata uvimbe katika njia ya haja kubwa na hivyo kupata maumivu wakati wa kujisaidia na haja yake mara nyingine huambatana na damu.
Aidha, anasema vyoo hivi pia vinaweza kuwa chanzo cha magonjwa yanayotokana na shambukizi katika utumbo mpana, kitaalamu ‘Inflammatory Bowel Disease’.
“Kila binadamu anapaswa kujisaidia na kuhakikisha haja yote imetoka na kwisha kabisa, inapobakia inaweza kusababisha maambukizi katika utumbo mpana kwa kuwa ule ni uchafu wenye mchanganyiko wa vitu vingi,” anasema Shita.
“Haja kubwa inapokuwa tayari imeshajitengeneza inapaswa kutoka yote, kama itabaki kipindi kirefu inaweza pia kuleta uambukizi katika utumbo mkubwa na hata katika kidole tumbo,” anasema Shita.
“Uchafu huu si tu unaweza kusababisha maambukizi, lakini pia unaweza kuwa chanzo cha saratani ya utumbo mkubwa. Wote tunajua kuwa mkusanyiko wa sumu mbalimbali mwilini unakuweka katika hatari ya kupata saratani, hivyo tatizo hili lisipotafutiwa ufumbuzi mapema linaweza kufikia huku,” anasema Shita.
Daktari Berko Sikirov kutoka Misri ambaye alifanyia utafiti matumizi ya vyoo vya kukaa anasema kuwa iwapo mtu ana tatizo la vivimbe vya ‘hemorrhoid’ linaweza kumalizika iwapo ataacha kutumia vyoo vya kukaa.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa tatizo hili linaweza kwisha kama litakuwa katika hatua za awali. Kwa wenye tatizo lililokomaa watalazimika kufuata matibabu kulingana na ukubwa wake.
Dk Sikirov anaongeza kuwa mbali na kupata vivimbe, pia mgonjwa anaweza kupata tatizo la kutokupata choo kwa muda mrefu.
Anabainisha kuwa kitendo cha haja kutoka kidogo na nyingine kubakia husababisha kuganda katika ukuta wa utumbo na zoezi hilo huendelea mpaka kuwa tatizo sugu.
“Haja kubwa huganda katika kuta za utumbo, hali hii huifanya haja izunguke kwa muda mrefu na ndiyo tatizo hili huanzia hapa,” anasema na kuongeza:
“Unapojisaidia ukiwa umekaa, ile njia ya haja kubwa huwa kama imejifunga, inabidi utumie nguvu nyingi sasa ukiwa na tatizo hili la kukosa haja kubwa huifanya itoke kwa uchache zaidi,” anasema Dk Sikirov.
Aidha, anasema kupata haja kubwa mara kwa mara ni muhimu kwa kuwa usipoitoa maana yake inazungusha sumu katika damu jambo ambalo ni hatari kwa afya.
Anaongeza kuwa kutopata haja kubwa ni kichocheo chenye uwezo mkubwa wa kusababisha saratani ya utumbo mkubwa na uambukizi katika kidole tumbo.
Tafsiri ya kitabibu inasema hali ya kukosa haja kubwa ni pale mtu anaposhindwa kuipata angalau mara tatu kwa wiki. Hata hivyo, ili ujue afya yako ni njema unapaswa kuwa unapata haja kubwa angalau mara moja kila siku.
Daktari Denis Burkitt aliwahi kuandika kitabu cha maelekezo ya chakula ili kuepuka ugonjwa wa saratani. Katika kitabu hicho alieleza namna ambavyo watu wanaweza kujikinga na saratani za aina mbalimbali.
Akizungumzia saratani ya utumbo mpana pamoja na kuelezea vyakula na aina ya maisha, pia aliwaasa watu kutumia choo cha kukaa ili kujiepusha na tatizo hilo.
Anaeleza kuwa kwa Marekani pekee, watu zaidi ya 150,000 hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa wa saratani ya utumbo mkubwa.
Mtaalamu wa Ngozi katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba Muhimbili (MUHAS), Profesa Kisali Pallangyo anasema matumizi ya vyoo hivyo yanaweza kuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa ya ngozi. Profesa Pallangyo anasema ni rahisi kuambukizwa magonjwa ya ngono na ngozi kwa urahisi pale unapotumia vyoo vya kukaa tofauti na vile vya kuchuchumaa.
Aidha, anayataja magonjwa yanayoweza kuwambukizwa kwa kutumia vyoo vya kukaa kuwa ni kaswende, harara, mba, kisonono, upele na mengine.
“Mtu mwenye magonjwa ya ngozi au ya ngono, anaweza kuyaacha katika ‘sink’ anapolikalia, hivyo ni rahisi kwa mtu mwingine ‘kuyachukua’ mara atakapokaa wakati wa kujisaidia,” anasema Prof Pallangyo.
Anasema vyoo hivi ni hatari kwa afya hasa pale vinapotumika katika jumuiya na kuongeza kuwa ni bora kutumia vile vya kukaa ili kujikinga na magonjwa.
Source: MWANANCHI