Like Us On Facebook

DAKTARI ADAIWA KUONDOKA NA VIFAA VYA ZAHANATI YA KIJIJI USIKU..

KATIKA hali isiyo ya kawaida, wananchi wa Kijiji cha Melela Wilaya ya Mvomero mkoani hapa, wamemtuhumu daktari wa zahanati ya kijiji hicho aliyetambuliwa kwa jina moja la Fulugesi kuondoka na vifaa vya upasuaji vyenye thamani ya mamilioni ya fedha. 
Tukio hilo limetokea hivi karibuni na kushuhudiwa na mwanakijiji Beatus Kanuti aliyemuona mtunza stoo wa zahanati hiyo, Mlelwa akitoa vifaa hivyo na kumkabidhi daktari huyo saa 5 usiku.
Jambo hilo lilichukuliwa kama ni wizi na kuwakamata watu hao wawili na kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji hicho.
Akihojiwa na Risasi Mchanganyiko, afisa mtendaji wa kijiji hicho, Bw. Fadhili Mwinyimvua alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. 
 “Ni kweli mwanakijiji Kanuti alimshuhudia daktari huyo akiondoka na vifaa 41 vya upasuaji usiku na kuvipeleka nyumbani kwake,” alisema mtendaji huyo. 
Mtendaji huyo aliongeza kuwa alipigiwa simu saa 5 usiku naye kuijulisha kamati ya ulinzi na usalama ya kijiji iliyoamua kukutana  na kwenda katika zahanati hiyo usiku huohuo.
Hata hivyo, mtendaji huyo wa kijiji alisema kuwa walipofika hawakumkuta daktari huyo na kuamua kumfuata nyumbani kwake na walipompekua walifanikiwa kuvikuta vifaa hivyo. 
Mtendaji huo ameongeza kudai kwamba, usiku huohuo wananchi wa kijiji hicho walipata taarifa na asubuhi waliandamana na kuitisha mkutano wa kijiji na uongozi wa serikali ya kijiji hicho kwa lengo la kujadili tukio hilo.
Katika mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita ndani ya ukumbi wa ghala la kuhifadhia chakula la kijiji, wanakijiji walimtaka mwenyekiti wao, Bw. Amiri Membe kumfikisha mahakamani daktari huyo vinginevyo watachukua hatua kali.
Juhudi za mwandishi wetu kuzungumza na daktari Fulugesi kuhusiana na madai hayo ziligonga mwamba licha ya mwandishi wetu kufika nyumbani kwake zaidi ya mara mbili.
Hata alipotafutwa kwenye zahanati hiyo hakupatikana na alipopigiwa simu iliita kwa muda mrefu bila kupokewa.
Daktari mmoja wa Zahanati hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake alikiri kutokea kwa tukio hilo.
Hata hivyo, muuguzi mkuu wa kijiji hicho, Kabendela, mlinzi wa zahanati Bw. Msosi na nesi wa zamu Bi. Mlaliki, Bw. Biatusi na afisa mtendaji walivihesabu vifaa vilivyopo katika zahanati hiyo na kugundua upungufu.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari