Na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Vitendo
vya ukatili dhidi ya watoto vimeendelea kushika kasi katika baadhi ya
maeneo hususani vijijini, licha ya Serikali na asasi mbali mbali
kulipigia kelele ambapo hivi karibuni Baba mmoja aliamua kuuza nyumba
ikiwa na watoto ndani na kutokomea kusikojulikana na kuwaacha wasijue la
kufanya.
Mkasa
huo wa ajabu ulitokea katika kijiji cha Hatwelo, Kata ya Ijombe Mbeya
Vijijini ambapo Mkazi huyo aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Yuta
alipouza nyumba yake na kutokomea yeye na mkewe na kuwaacha watoto
wawili wenye umri kati ya miaka 9 na 11 wakikosa mahala pa kuishi.
Akizungumzia
sakata hilo kijijini hapo, Mwanaharakati wa haki za Binadamu, Yasin
Yuta, alisema majirani waligundua baada ya kusikia kelele za mtoto mmoja
aliyefahamika kwa jina la Erasto Emmanuel (11) aliyekuwa amefungiwa
ndani na kukaa kwa siku saba.
Alisema
baada ya kumfungulia mtoto huyo ndipo ilipobainika kuwa nyumba hiyo
ilikuwa imeshauzwa huku mtoto akiwa ndani na ndipo mnunuzi alipofunga na
kufuli bila kujua kama kuna mtoto ndani huku watoto wengine wakiwa kwa
ndugu zao ambao pia hawakuelezwa kama nyumba imeuzwa.
Nyumba
hiyo iliuzwa kwa Dati Nsagaje kwa gharama ya shilingi 750,000/= ikiwa
ni nyumba mbili pamoja na kiwanja ambapo mnunuzi huyo alilipa kianzio
cha shilingi laki nne biashara iliyofanyika tangu April 26 mwaka huu na
kiasi kilichobaki wakiwa wameahidiana kulipana Mwezi Mei 15, Mwaka huu.
Wahanga
wa tukio hilo ambao ni watoto walisema hawakuwa na taarifa zozote za
kuuzwa kwa nyumba wanayokaa ambapo walisikia kuwa baba yao ameenda
Sumbawanga kumfuata mke wake ambaye inasemekana aliolewa na mwanaume mwingine.
“
Nilikuwa nimelala ndani ambapo nilipoamka asubuhi nilikuta mlango
umefungwa kwa nje hata hivyo nilivumilia hadi njaa ilipoanza kuniuma
baada ya siku tano nikaanza kupiga kelele ndipomajirani walipokuja
kunifungulia na kuniambia nyumba imeuzwa” alisema mtoto Erasto Emmanuel.
Mtoto
mwingine aliyetelekezwa ambaye siku ya tukio alikuwa ameenda kulala kwa
bibi yake Groli Emmanuel (9) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi
Hatwelo alisema siku akiwa anaondoka aliagwa na baba yake ambaye
alimwachia shilingi 3000 lakini hakumwambia kama nyumba imeuzwa.
Kutokana
na kitendo hicho kutokukubalika,baadhi ya majirani
walisema ni kitendo cha kinyama na hakipaswi kufumbiwa macho ambapo
waliamua kuchanga fedha ili kuikomboa nyumba ili irudi mikononi mwa
watoto.
Majirani
hao walifanikiwa kuchanga shilingi 410,000/= alizokuwa amedai mnunuaji
ili aweze kurejesha nyumba ikiwa ni fedha alizokuwa ametoa awali hivyo
kukubaliana kuicha nyumba hiyo ambayo kwa mujibu wa majirani na baadhi
ya ndugu wamesema itakuwa ni mali ya watoto.
Hata
hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida na kuonesha kukosa uwajibikaji
kwa baadhi ya viongozi wa Serikali ya Kijiji ambao walishiriki moja kwa
moja zoezi hilo huku wakiwa wamesaini kama mashahidi na kugonga mhuri wa
Serikali ya Kijiji walipoulizwa kuhusiana na sakata hilo hawakuwa na
majibu ya kuridhisha.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Hawelo, Ibrahimu Mponzi, alisema kitendo alichokifanya
muuzaji ni cha kawaida kwa sababu ameuza mali yake mwenyewe na kwamba
wao kama majirani na serikali ya kijiji hawawezi kuhoji atakako waacha
watoto kwa sababu ni mipangilio ya maisha ya kila mtu.
Mbali
na mwenyekiti wa Kijiji kuwa shahidi wa upande wa mnunuaji akiwa
sambamba na watu wengine wanne akiwepo Mkewe ambaye pia ni Balozi wa
nyumba kumi pia waliosaini wengine ni ndugu wa mnunuaji ili hali muuzaji
akiwa hana shahidi hata mmoja.
Aidha
juhudi za majirani kuikomboa nyumba hiyo na kuwa mali ya watoto
zilifanikiwa ambapo mnunuzi Datistani Mwanshinga alibatilisha ununuzi wa
nyumba hiyo Mei 9, Mwaka huu baada ya kukiri kurejeshewa fedha zake.