Stori: MWANDISHI WETU
MATUKIO na vitendo viovu vinaendelea kushamiri juu ya uso wa nchi! Kijana anayedaiwa kuwa muumini wa kanisa la kilokole (jina tunalo) la jijini Dar, Faraji Oti amekutwa na mazito akidaiwa kufumaniwa na mke wa mtu aliyetajwa kwa jina moja la Jesca..
MANZESE, DAR
Tukio hilo lililoongeza furaha ya Shetani, lilichukua nafasi mwanzoni mwa wiki hii majira ya 11:00 jioni huko Manzese, jijini Dar.
Kwa mujibu wa watu wa karibu na wahusika hao, kisa kilianzia kwenye simu ambapo mwenye mke alidai kunasa mawasiliano ya jamaa huyo na mkewe.
Ilidaiwa kuwa ukaribu wa wawili hao ulianzia kwenye kwaya waliyokuwa wakiitumikia kisha kuzua mawasiliano tata.
OTI AONYWA
Habari zilidai, kuna wakati mume wa Jesca alimuonya Oti kukaa mbali na mkewe lakini jamaa alipuuza huku akidaiwa kutoa maneno makali na ya dharau kwa mwenye mali.
“Jamaa alikuwa akimuonya sana, lakini aliambulia matusi na kejeli, mwisho wa siku imekuwa hivyo na jamaa akawa hana la kujitetea,” alidai mmoja wa watu wa karibu na mwenye mke.
SIMU NI TATIZO?
Habari zilizidi kudai kuwa siku ya tukio mwanamke huyo alianza kutuma meseji kwa jamaa ya kumjulia hali na kuiacha simu mbele ya mumewe aliyejulikana kwa jina moja la Mustapha.
Ilisemekana kuwa mwenye mke aliamua kuendeleza mawasiliano hayo akijifanya Jesca na ndipo jamaa akaingia ‘kingi’, akapanga wakutane bila kujua aliyekuwa akibadilishana naye sentensi kwa njia ya meseji ni ‘mume mwenzie’.
Ilidaiwa kuwa ili kumshikisha adabu Oti, alimbana mkewe na kumwambia, pona yake afanikishe kupatikana kwake.
Kulinda ndoa yake, mke aliamua kuendelea kuchati na Oti na wakapanga wakutane na baada ya hapo mume akafuatilia kwa nyuma hadi wawili hao walipokutana maeneo ya Manzese.
Ilidaiwa kuwa, baada ya Oti na Jesca kuingia kwenye gesti iliyopo maeneo hayo, jamaa huyo aliwajulisha marafiki na watu wake wa karibu ambao walifika eneo la tukio na kuwakuta wakijiandaa ‘kufanya yao’.
Habari ziliendelea kutapakaa kuwa Oti hakuwa na cha kusema zaidi ya kujitetea huku akiomba msamaha kwa madai ya kupitiwa na shetani.
Ilisemekana kuwa jamaa mwenye mke alimuamuru Oti aondoke zake huku washikaji wakimnyang’anya simu.
Baada ya kuzinyaka taarifa hizo, mwanahabari wa gazeti hili alitumia njia ya ‘kiitelejensia’ kuipata namba ya simu ya mtuhumiwa ambapo alipopigiwa alikiri kukutwa na masaibu hayo huku akijitetea kuwa hakuwa na uhusiano mbaya zaidi ya mazungumzo ya kawaida na kuomba msamaha kwa yote yaliyotokea.
“Ni kweli nilikutana na yule mwanamke lakini sikuwa na nia ya kufanya chochote naye, japo tuliwahi kuwa wapenzi siku za nyuma, pamoja na hayo sina jinsi zaidi ya kukiri na kuomba msamaha, nilishatubu kwa Mungu wangu,” alisema Oti na kuongeza:
“Narudia tena ndugu mwandishi, sina uhusiano mbaya na Jesca kwani hata siku hiyo nilikuwa na lengo la kusalimiana naye tu na si kufanya chochote kibaya.”
MASWALI TATA
Kama Oti alimwita mwanamke huyo kwa ajili ya salamu na mazungumzo ya kawaida mbona walikutwa chumbani?
Kama kweli Mustapha alikuwa na nia ya kumpata mbaya wake na kumchukulia hatua za kisheria kwanini hakuvihusisha vyombo vya usalama?
Ikiwa Jesca ana mume aliwezaje kumtumia meseji mpenzi wake wa zamani na baadaye kushiriki katika mtego?
Mezani kwa mhariri
Ijumaa linaendelea kuifanyia kazi habari hii na chochote kipya kitakachopatika tutawaletea.
-IJUMAA VIA GPL