Maelfu wakazi wa jiji la Dar es salaam wengi wao wakiwa ni wafuasi wa vyama vya Chadema ,Cuf na NCCR Mageuzi wemefurika katika viwanja vya jangwani kuwasilikza viongozi wakuu wa vyama hivyo ambapo kwa pamoja viongozi hao wanapinga hatua ya serikali kuingiza baadhi ya vipengele katika mswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba .
Viongozi hao wanadai kuwa vipengele hivyo vitapelekea kupatikana kwa katiba ya upande mmoja na kuongeza kuwa kama mswada huo hautafanyiwa marekebisho, basi wao hawatashiriki katika bunge la katiba.
Katika viwanja hivyo ulinzi uliimarishwa kutoka katika vikundi mbalimbali vinavyomilikiwa na vyama hivyo huku shamra shamra za huko na kule zikiwa hazikosekani ili mradi kunogesha mkutano.
Mwenyekiti wa taifa wa Chadema na ambaye ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Mh Freeman Mbowe amewataka watanzania kuacha uoga na wasimame imara kudai katiba bora.
Naye mwenyekiti wa Cuf Mh Profesa Ibrahim Lipumba amesema Tanzani inahitaji katiba ambayo italinda na kusimamia rasilimali za taifa kuweza kutimia kwa usawa na kuzingatia mahitaji ya watanzania wenyewe.