Taarifa hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Zuberi Samataba, alipokuwa akizungumza na MTANZANIA.
“Siyo kweli hata kidogo, mitihani aliyokuwanayo Mbatia ni feki na haikufanywa na wanafunzi wa darasa la saba kama alivyosema.
“Sisi hatujui Mbatia aliipata wapi hiyo mitihani, halafu wizara haitungi mitihani bali mitihani inatungwa na NECTA, mitihani ile ilitungwa ikiwa ni programu maalumu ya kupima uelewa wa wanafunzi wa darasa la saba na sio moko kama alivyosema.
“Pili ni kwamba, Mbatia alipoiona ile mitihani angefanya jambo la busara kuwasiliana na sisi kwa ajili ya kujiridhisha kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari, kwa sababu tungemueleza ukweli, kwamba mitihani aliyokuwa nayo ni feki na haijafanywa na wanafunzi wa darasa la saba,” alisema Samataba.
Alisema kwamba, hata Kamishina wa Elimu wa wizara hiyo, Profesa Ellustela Bhalalusesa, amelitolea ufafanuzi suala hilo kwamba mitihani iliyotajwa na Mbatia ilikuwa feki.
“Kamishina kalizungumzia hilo na mimi narudia kulizungumzia, kwamba mitihani hiyo ilikuwa feki, sasa wewe mtafute Mbatia umuulize mitihani hiyo aliipata wapi maana iko tofauti kabisa na ile tuliyowapa wanafunzi wa darasa la saba kuifanya,” alisema.
Majibu hayo, yamekuja ikiwa ni siku chache tangu wizara hiyo izindue Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), katika sekta ya elimu na kujiwekea mikakati tisa ya kuitekeleza.
Mbatia alipotafutwa ili aweze kutoa ufafanuzi juu ya mitihani hiyo, hakupatikana.
Akizungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam hivi karibuni, Mbatia alisema ameibua madudu mapya ya elimu katika mitihani ya Hisabati, Kiswahili na Kiingereza.
Aliyataja madudu hayo katika mitihani hiyo kuwa, katika Somo la Kiswahili na Kiingereza, kulikuwa na makosa ya kisarufi wakati katika Hisabati kulikuwa na maswali yasiyokuwa na majibu.
Alisema aliupeleka mtihani wa Hisabati uliofanywa na wanafunzi hao katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kumkabidhi profesa mmoja (hakutaka kumtaja jina), ambapo aliufanya na kukuta kuna maswali mengine hayakuwa na majibu kwa sababu yalikosewa.
Aidha, alisema katika mtihani wa Kiingereza na Kiswahili uliokuwa na makosa makubwa ya kisarufi, aliupeleka katika Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu hicho, ambapo wasomi hao walisikitishwa na makosa yaliyokuwa katika mitihani hiyo.
Kutokana na madudu hayo, alipendekeza Serikali iunde Tume ya Kudumu ya Elimu itakayokuwa na hadidu za rejea 12, mojawapo ikiwa ni kushughulikia ubora wa elimu na kudhibiti mambo yote yanayosababisha kutetereka kwa ubora huo.