Kiukweli hili ni tatizo sugu ambalo linaepukika lakini kuna ugumu kidogo katika kuliepuka moja kwa moja. Mitaani tunapoishi wapo wanaume ambao wasione msichana mrembo akipita, lazima wataanza kumsumbua kwa kumuita na wengine kufikia hatua ya kuwatomasa tomasa sehemu zao nyeti bila ridhaa yao. Mbaya zaidi ni kwamba wanaume hao hufanya hivyo hata kwa wanawake ambao ni wake za watu au wenye wapenzi wao.
Tabia hii huwakera sana baadhi ya wanawake hasa wale wanaojiheshimu na kuziheshimu ndoa na uhusiano wao. Hata hivyo, ili kuwaepuka wanaume wakware wakati mwingine huwa ngumu kwa kuwa wengi wao hawana akili timamu, muda mwingi wao huwaza kufanya ngono tena na kila mtu watakayemuona bila kufikiria madhara wanayoweza kuyapata baadaye.
Niseme tu kwamba, wanaume wa aina hii wapo wengi ila kwa mwanamke anayeiheshimu ndoa yake au uhusiano wake na akaweka nia ya kuwaepuka, inawezekana! Hizi hapa chini baadhi ya njia muhimu za kukabiliana na tatizo hilo la kusumbuliwa hivyo na wanaume.
MAVAZI YAKO YAKOJE?
Wanawake wengi sana hukosea katika suala zima la uvaaji. Baadhi yao hupendelea kuvaa mavazi yanayoonesha maungo yao kiasi cha baadhi ya wanaume kuwachukulia kuwa ni machangudoa.
Ni kweli kwamba mavazi ya mtu hayawezi kumfanya akaingizwa katika kundi la watu fulani na pia kila mtu anao uhuru wa kuchagua avaeje lakini, kwa uhalisia mwanamke asiyeujali mwili wake kwa kuvaa nguo zisizokuwa na heshima, asitarajie kuuepuka usumbufu wa wanaume wapenda ngono. Ni lazima watamtongoza na wakati mwingine kumfanyia vitendo vya kumdhalilisha.
Hivi mwanamke kuvaa ‘kitop’ na suruali inayobana huku ikionesha shepu ya sehemu zako nyeti kisha kukatiza mbele za wanaume kutakuwa kunamaanisha nini kama siyo kujitangaza kwao? Hivi kwa mavazi hayo utakuwa na tofauti gani na wale wanaoijiuza kule Ohio?
Ifike wakati uondokane na ulimbukeni wa kwenda na wakati hasa kwa wewe mwanamke ambaye umeolewa ama una mpenzi wako. Vaa mavazi ya heshima kila unapokwenda.
Mavazi yanayoonesha maungo yako yavae ukiwa na mpenzi wako chumbani. Naamini kwa kuvaa hivyo, kidogo utakuwa unapunguza ile kasi ya wanaume wakware kukusumbua.
TABIA ZAKO VIPI?
Baadhi ya wanawake acha wasumbuliwe kwani tabia zao huwafanya wasiheshimike mbele ya jamii na kuonekana kwamba ni jalala. Unakuta mwanamke anapita mbele za wanaume kisha anatembea kwa kujishebedua huku akitingisha maungo yake makusudi, hapo unatarajia nini?
Achilia mbali hilo, wapo baadhi ya wanawake ambao ni rahisi kuchukuliwa na wanaume. Yaani hawawezi kusema hapana! Ukiwa na tabia hiyo tambua kuwa, kila mwanaume mkware atataka kuweka mhuri wake mwilini mwako.
USITANIANE NA WANAUME!
Wanawake wengine ni wa ajabu sana. Unamkuta anajenga ukaribu sana na baadhi ya wanaume na kufikia hatua ya kutaniana nao katika mambo ambayo mwishowe huwa kutongozana.
Mwanamke aliyeolewa ama mwenye mpenzi wake hatakiwi kujenga ukaribu sana na wanaume wa pembeni. Unapopita maskani wamekaa wavulana, wasalimie kisha chukua hamsini zako, utani wa kijinga epukana nao kwani mwishoni watakutongoza na ukionesha kuchukia watadai walikuwa wanakutania kumbe wako ‘sirias’.
MWAMBIE MPENZI WAKO
Sishauri kila mwanaume atakayekuchomekea umwambie mpenzi wako. Nasema hivyo kwa kuwa, natambua itageuka kero kwa mwenza wako. Ila sasa wapo wanaume ambao ni ving’ang’anizi. Unamweleza kuwa una mpenzi wako lakini hakuelewi ni vema ukamtaarifu mumeo ili akae akijua.
Hiyo itasaidia sana kwani mumeo anaweza kuchukua hatua zinazostahili dhidi yake na hatimaye kuweza kupunguza kasi ya usumbufu huo. Kamwe usithubutu kukaa kimya. Mbaya zaidi ni kwamba unaweza kukuta shemeji yako ambaye ni rafiki wa karibu wa mpenzi wako ama mwanaume anayemfahamu vilivyo mumeo akakutongoza!
Huyu ni hatari sana na wala usisubiri akutongoze mara mbili. Siku ya kwanza tu atakayokutamkia maneno yake ya kipuuzi, kwanza geuka mbogo, mkaripie kwa ukali kisha mpe taarifa mpenzi wako.
Wanaume wa siku hizi wametawaliwa na tamaa zisizokuwa na msingi. Ukitaka wakusumbue watakusumbua kweli na wakati mwingine wanaweza kukushawishi ukamsaliti mpenzio wako.
Kikubwa ni mwanamke kuwa na msimamo. Kutokukubali kugeuzwa kiti cha daladala, kwamba kila mtu anaweza kumchezea. Naamini msimamo huo pamoja na mambo hayo niliyoyataja hapo juu unaweza kuepukana na usumbufu huo kutoka kwa wanaume.