Banda alitoa pongezi hizo jana wakati akihutubia Mkutano wa 33 wa Wakuu wa SADC baada ya kukabidhiwa nafasi ya uenyekiti wa jumuiya hiyo kutoka kwa Rais wa Msumbiji, Dk Armando Guebuza.
“Wananchi wa Malawi, mimi na SADC tunampongeza Kikwete kwa kuimarisha amani, demokrasia na usalama katika jumuiya katika kipindi chake cha uongozi (wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama),” alisema.
“Pia Rais wa Msumbiji, Armando Guebuza katika uongozi wake wa uenyekiti alishirikiana na Kikwete kushughulikia matatizo ya kisiasa na kuufanya ukanda wa nchi za SADC kuwa na amani,” alisema Rais Banda, ambaye nchi yake ina mgogoro na Tanzania juu ya mpaka wa Ziwa Nyasa.
Mgogoro huo uliibuka baada ya Serikali ya Malawi bila kushauriana na Tanzania, kutoa leseni kwa kampuni mbili za kigeni, kutafuta mafuta katika eneo la Ziwa upande wa Tanzania.
Chanzo cha mgogoro huo unaoshughulikiwa na jopo la marais wastaafu wa Afrika; Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Joachim Chisano (Msumbiji), Festus Mogae (Botswana) na wanasheria saba wa kimataifa, ni mikataba yenye utata iliyoachwa na wakoloni.
Sifa za Kikwete
Katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa Rais Kikwete katika asasi hiyo ya siasa, ulinzi na usalama aliweza kufanikisha kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Zimbabwe, ambao Robert Mugabe ameshinda.
Amefanikisha pia kuanza kwa mchakato wa amani na kupatikana kwa muafaka wa kisiasa nchini Madagascar.
Pia katika kipindi chake, alifanikisha kupelekwa kwa wanajeshi wa kulinda amani katika mji wa Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambapo waasi wa M23 wanapambana na wanajeshi wa serikali. Wanajeshi hao wa kulinda amani wametoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.
Rais Kikwete amekabidhi madaraka hayo jana kwa Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba. Banda aahidi amani Akizungumzia mkakati wake wakati wa uongozi wake wa mwaka mmoja kama Mwenyekiti wa SADC, Banda alisema ili ukanda wa SADC uwe na amani na usalama ni lazima nchi wanachama zipambane na umasikini.
“Lazima tuimarishe siasa za ndani za nchi zetu, tuwe wavumilivu wa kisiasa na tusaidie wanawake wasiwe nyuma,” alisema. Aliahidi kuimarisha jumuiya za kikanda pamoja na kilimo kwa maelezo kuwa kilimo ndicho mwajiri mkuu wa wananchi wa nchi za SADC.
“Nitahamasisha kilimo kiboreshwe ili wananchi wa SADC waweze kuendesha kilimo cha biashara na pia sekta binafsi waingie kwenye kilimo na tupate masoko mapya ya bidhaa za kilimo nje ya mipaka ya ukanda wetu”.
Alitaka katika ukanda wa jumuiya ya SADC kuboreshwe mwingiliano wa wananchi wa nchi za ukanda huo. Alisema haiwezekani kuboreshwa kwa jumuiya za kikanda bila kuruhusu mwingiliano huru wa wananchi wake.
Rais Banda alitaka wanawake wapewe nafasi katika uongozi na kujengewa uwezo katika kuimarisha uchumi na kuondokana na umasikini na kusisitiza kuwa, “wanawake ndiyo wanaopambana na umasikini, wanabakwa, wanakabiliwa na unyanyasaji na wengi wamepoteza utu wao”.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Dk Nkosazana Dlamini- Zuma alizitaka nchi za Afrika kuimarisha miundombinu ili mazao ya wakulima yaweze kusafirishwa pamoja na kuboreshwa kilimo, uwekezaji na kujengwa kwa viwanda.
“Lazima tufanye kazi pamoja kuwahakikishia chakula watu wetu wa SADC na Afrika haiwezi kuendelea bila kuweka wanawake kila maeneo na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazotukabili za tatizo la ajira kwa vijana, umasikini, sekta duni ya viwanda na tatizo la kutokuwepo usawa wa kijinsia,” alisema Zuma