Aliyekuwa rais wa marekani Bill Clinton amempongeza rais wa Rwanda Paul Kagame kwa mafanikio ya nchi yake licha ya madai kwamba amekuwa akiunga mkono makundi ya waasi katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo yanakiuka haki za kibinadamu.
Bwana Clinton amesema katika mahojiano na BBC kwamba madai hayo ambayo Rwanda inayakataa hayajathibitishwa mahakamani.
Pia alisema kuwa kuna changamoto kubwa katika mpaka wa Rwanda na Congo, kwani una watu chungu nzima ambao walihusika na mauaji ya halaiki miaka ya tisini.
Lakini bwana Clinton amesema kuwa anathamini serikali ya Rwanda kutokana na mafanikio ya kiuchumi yalioafikiwa chini ya rais Kagame.
Kiongozi huyo amekuwa akizuru mataifa ya Afrika pamoja na mwanawe Chelsea ili kujionea miradi ya wakfu wake.